Leila Rashid |
Malkia Leila Rashid kutoka bendi la jahazi ni mja
mzito.
Ni mkewe Mfalme Mzee Yussuf, Mama ya watoto wawili na
msanii nyota katika tasnia ya taarab.
Bi. Leila anaelezea historia yake katika sanaa ya
burudani na maisha yake binafsi.
“NILIANZA kumfahamu Mzee Yusuf katika ukumbi wa Equator
Grill uliopo Mtoni kwa Azizi Ally, Temeke, Dar es Salaam.
Nilipenda sana jinsi alivyokuwa anapiga kinanda wakati
huo, ” anasema Bi. Leila Rashid.
Anasema kipindi hicho alikuwa akihudhuria maonyesho
mbalimbali yaliyokuwa yakifanywa na kikundi cha taarab cha Zanzibar Stars,
ambacho Mzee Yusuf alikuwa mmoja wa wasanii wake, akiwa anapiga kinanda.
Leila, ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa mwimbaji tangu
akiwa mdogo anasema, alikuwa na kawaida ya kwenda kwenye ukumbi huo kila
Zanzibar Stars ilipokuwa ikifanya onyesho.
“Nilikuwa na ndoto ya kuimba taarab tangu nilipokuwa
mdogo na nilikuwa nikivutiwa sana na uimbaji wa Sabah Salum ‘Muchacho’ kutokana
na uimbaji wake mzuri,” anasema.
Leila anasema alikuwa akitumia muda mwingi akiwa
nyumbani kwao kuimba nyimbo mbalimbali za waimbaji nyota wa muziki huo kwa
lengo la kupima uwezo wake kama anaiweza fani hiyo.
Mwimbaji huyo mwenye sura na umbo la kuvutia, anasema
siku ya kwanza kuanza kufahamiana na Mzee Yusuf, alijihisi mwenye furaha kubwa.
“Kwa kweli siku ya kwanza kufahamamiana na Mzee Yusuf
nilijihisi mwenye furaha sana na niliamini ataweza kunisadia kukuza kipaji
changu cha uimbaji nilichokuwa nacho,” anasema.
Baada ya kufahamiana na kuwa karibu na Mzee Yusuf,
Leila anasema mwimbaji huyo gwiji wa taarab alimshawishi ajiunge na kikundi cha
Zanzibar Stars, ambacho kilikuwa kikiwika wakati huo.
Leila, ambaye kwa sasa anasikika kila kona ya nchi
kutokana na uimbaji wake mzuri, anasema ushauri aliopewa na Mzee Yusuf
aliusikiliza na kuufanyia kazi.
Anasema alijiunga na Zanzibar Stars miaka tisa
iliyopita na wimbo wake wa kwanza ndani ya kikundi hicho unajulikana kwa jina
la ‘Riziki atoae Mola’.
Mwimbaji huyo mwenye bashasha anasema, baada ya
kurekodi wimbo huo, hakufanikiwa kutoa wimbo mwingine kutokana na ubinafsi
uliokuwepo katika kundi hilo.
Anasema mara yake ya kwanza kupanda kwenye steji
alikuwa na hofu, lakini alifanikiwa kuimba vizuri na kushangiliwa na mashabiki
wengi.
Leila, mwimbaji mwenye sauti nyororo na macho ya
kuvutia anasema, aliamua kuondoka Zanzibar Stars kutokana na sababu mbalimbali,
ikiwemo ubinafsi na uchache wa maslahi.
Anasema licha ya kwamba kipindi hicho Zanzibar Stars ilikuwa inatamba kwa nyimbo
za taarab, maslahi yalikuwa madogo, hali iliyosababisha waimbaji wengi mahiri
kuhama.
Mwimbaji huyo anasema, mwaka 2006 alijiunga na kundi
jipya la Jahazi Morden Taarab ‘Wana wa nakshinakshi’ chini ya Mkurugenzi wake
Mzee Yusuf.
Anasema kuanzishwa kwa kundi hilo, ambalo linaongozwa
na mume wake, Mzee Yusuf kulimfanya afahamike ndani na nje ya nchi ya Tanzania.
“Jahazi ndiyo imenifanya nifahamike kila kona ya nchi
hii, nadhani kama si kundi hili, hadi sasa ningekuwa sifahamiki,” anasema.
Leila anasema wimbo wa ‘Maneno ya mkosaji’, ambao
ulikuwa wa kwanza kuimba katika kundi hilo, ulimpandisha chati na kumpa
umaarufu mkubwa na kusisitiza kuwa, kwa sasa anajiona yupo kwenye chati ya juu.
“Sidhani kama kuna mwimbaji anayeweza kujaribu kusimama
na mimi kwa sasa, niko juu na nimeiva kila idara,” anajigamba mwimbaji huyo.
Mwimbaji huyo anasema, haoni tatizo kufanyakazi katika
kundi moja na mumewe kwa sababu ameshaizoea tabia ya mumewe.
Leila anasema ataendelea kuheshimiana na mume wake kwa
kipindi chote watakachoendelea kuwa pamoja huku akisisitiza kuwa, hakuna
anayeweza kuwatenganisha kwa vile anampenda kuliko kitu kingine chochote.
“Nampenda sana mume wangu ndio maana hata anapotaka kuoa mke mwengine, huwa
nampa ruksa kwani najua kufanya hivyo ni sheria kwa mujibu wa dini yetu,”
anasema.
Leilah, ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wa ‘Sina Mda
huo’, amekitaja kibao cha ‘Kwa hilo hujanikomoa’ kuwa ndicho kilichomfanya
apendwe zaidi na mashabiki kutokana na kukiimba kwa umahiri mkubwa.
Additional information via RUSHA ROHO Blog....
No comments:
Post a Comment