Malkia wa Mipasho Bi. Khadija Kopa |
Big Daddy A.K.A Mfalme Mzee Yussuf |
Imebainika wazi kuwa mambo sio shwari kati ya Malkia wa
Mipasho Bi. Khadija Kopa na Big Daddy Mfalme Mzee Yussuf katika ulimwengu wa
taarab.
Akithibitisha hayo katika ziara yake hapa mjini
Mombasa, Bi. Khadija alisema binafsi ameshangazwa na kukerwa zaidi na kundi la
Jahazi kutokana na vitendo wanavyomfanyia.
Alisema baadhi ya waimbaji na viongozi wa kundi hilo
wamejenga chuki za wazi wazi dhidi yake, bila sababu yoyote, hali inayompa wakati
mgumu.
Khadija alisema mara kadhaa anapoalikwa kufanya
maonyesho kwa kushirikiana na kundi hilo, viongozi na wasanii wake humfanyia
vituko vya kila aina, ambavyo humfanya wakati mwingine ashindwe kuimba.
"Mara kwa mara ninapoalikwa kuimba pamoja na
Jahazi, huwa sipewi ushirikiano. Hunifanyia vituko vingi sana,”alisema.
Mkongwe huyo wa mipasho alisema binafsi hana bifu na
uongozi ama msanii yeyote wa kundi hilo na kwamba anawaheshimu.
Pia Khadija alidokeza kuwa , kutokana na vituko
anavyofanyiwa na uongozi wa kundi hilo, analiona kama vile limeamua kumdhalilisha
na kumvunjia heshima.
Akitoa mfano alisema, katika tamasha la Mitikisiko ya
Pwani lililofanyika mwishoni mwa mwaka jana katika ukumbi wa Diamond Jubilee,
Dar es Salaam, huko Tanzania alilazimika kuimba kwa tabu baada ya Jahazi
kuondoa stejini baadhi vyombo vyao.
Kwa mujibu wa Khadija, kuna siku alikodiwa na
mfanyabiashara Abbas Shentemba kuimba akiwa na waimbaji wengine pamoja na kundi
la Jahazi, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kuwekewa ngumu na
viongozi wa kundi hilo.
"Nakumbuka nilialikwa pamoja waimbaji wengi,
akiwemo Mohamed Iliyas na Afua Suleiman, lakini sikuweza kuimba kutokana na
kubaniwa na uongozi wa Jahazi na kila nilipokuwa namkumbusha msimamizi wa
onyesho hilo, alinijibu kwa kejeli,”alisema.
"Alianza kupanda jukwaani Afua, wakati anapanda
Mohamed Iliyas, nilimtuma mpiga kinanda mmoja wa Jahazi akamwambie yule
msimamizi kwamba akiteremka Iliyas nipande mimi, lakini wakampa majibu ya
kebehi,”aliongeza.
Akisimulia zaidi mkasa huo, nguli huyo wa mipasho
alisema, siku hiyo alipata taarifa mapema kwamba hawezi kuimba na alimfuata
aliyemkodi na kumuuliza, lakini alimpa majibu kwamba lazima aimbe.
Alisema baada ya Iliyas kuteremka stejini, alipanda
Mzee Yusuf na kuanza kuimba na hapo ndipo alipoamini maneno aliyoambiwa mapema
kwamba hawezi kuimba siku hiyo.
“Baada ya Mzee Yusuf kupanda stejini, nilimfuata
aliyenialika na kumuaga na yeye akakubali, kwa maana hiyo niliondoka bila
kuimba,”alisema Khadija.
"Mimi binafsi ni mtu wa watu, kwa hiyo naomba kama
Jahazi nimewakosea kitu, wanambie ili niwaombe radhi na mimi kama wamenikosea
waniombe radhi,”aliongeza.
"Namheshimu kila mtu,
sijawahi kugombana na yeyote, naona Jahazi wanajisumbua kwa sababu kwangu ni
watoto wadogo sana," alisema.
Additional information Via RUSHA ROHO Blog...
Additional information Via RUSHA ROHO Blog...
No comments:
Post a Comment