Sunday 2 December 2012

BENDI LA JAHAZI LAKAMILISHA ALBUM YAO MPYA KWA JINA LA 'WASIWASI WAKO NDIO MARADHI YAKO'........................

Bendi la Jahazi chini ya uongozi wake Mfalme Mzee Yussuf limekamilisha album yao mpya kwa jina la 'Wasiwasi wako ndio maradhi yako.'

Akizungumza kwa njia ya simu na blog hii, Big Daddy Mfalme Mzee Yussuf amethibitisha hayo na kudokeza kuwa album hiyo huenda ikatambulishwa huko Mombasa na Nairobi Kenya mwezi huu wa disemba endapo bendi hilo litapata udhamini.

Pia Mzee Yussuf alifichua kuwa album hiyo itazinduliwa rasmi tarehe 31 mwezi huu wa disemba katika shamra shamra za kukaribisha mwaka mpya wa 2013 huko Dar es Salaam Tanzania.

Hapo awali, Mzee Yussuf alikariri kuwa album hiyo itakuwa na vibao sita ikiwemo kibao kitakachobeba jina la album hiyo kwa jina la 'Wasiwasi wako ndio maradhi yako' itakayoimbwa naye Mzee Yussuf miongoni mwa vibao vingine vitakavyowashirikisha wasanii mbali mbali wa bendi hilo akiwemo Rahma Machupa, Mtoto pori Moh'd Ali, Fatma Ali, Malkia Leila Rashid na Chiriku Original Khadija Yussuf.

Huku hayo yakijiri…….Bendi linalokuja kwa kasi sana nchini Tanzania la T Moto linajiandaa kuachia album yake ya tatu kwa jina la ‘Kama kupendwa ni hatia magereza yangejaa’ baada ya kukamilisha album yao ya pili ya ‘Domo la Udaku.’

Kulingana na mkurugenzi wa bendi hilo Amin Salmin, album hiyo itakuwa na vibao kadhaa ikiwemo kibao kwa jina la ‘Kuna Mungu sio Miungu’ kitakachoimbwa na Tabasamu la kumwaga Bi. Jokha Kassim na baadhi ya mashairi katika kibao hicho ni kama yafuatayo,.... 

'Unalolitaka mlimwengu haliwezi kunifika, Kuna Mungu sio miungu, Mungu hana mshirika, Nakueleza hilo ufahamu, Bure unahangaika mwenzangu, Hayaingiliwi na mwanaadamu mamlaka ya Mwenyezi Mungu.' 

“Album hiyo inaandaliwa kwa sasa na tutawashirikisha wasanii wapya kutoka bendi tofauti tuliotia nao mkataba japo kwa sasa majina yao nitayabana lakini nitawajulisha wakati mwafaka utakapowadia,” Akasema Amin Salmin.

Haya yanajiri baada ya bendi hilo kujikakamua baada ya kukumbwa na changamoto kadhaa katika siku za nyuma na kulipelekea kusambaratika baada ya kutambulisha album yao ya kwanza ‘Aliyeniumba hajanikosea.’

No comments:

Post a Comment