Monday 17 December 2012

WAGOMBANO NDIO WAPATANO??????

Waambiwa ndugu wanapogombana shika jembe ukalime, wakipatana nenda ukavune... na kwa mara nyengine tena huenda mambo sio shwari kati ya mtu na nduguyee yaani Sauti ya Chiriku Bi. Khadija Yussuf na Big Daddy Mfalme Mzee Yussuf.

Akihojiwa kupitia kipindi cha ‘Sham Sham za Pwani’ kinachorushwa kupitia runinga ya ITV, Bi. Khadija Yussuf aliangua kilio akidai kuna ‘Vidudu watu’ ndani ya bendi la jahazi wanaopeleka maneno ya urongo kwa kaka yake ili kuwagombanisha kiasi cha kuwafanya wasielewane vizuri.

Alipoulizwa ni kitu kipi kinachomkera katika maisha yake.... Naye (Khadija Yussuf) bila kutafakari kwa muda mrefu alijibu kuwa, ni kile kitendo cha mtu kutoka aendako na kwenda kumzushia maneno ya uongo kwa Mzee.
 

"Kinachoniuma zaidi ni kwamba afadhali hayo maneno ningekuwa nimeyasema, lakini sijafanya hivyo, Hawa watu wanapaswa kutambua kwamba kuna Mungu na mimi na Mzee Yussuf tumezaliwa baba mmoja mama mmoja, atakapozikwa Mzee Yussuf ndipo nitakapozikwa mimi,"alisema Khadija huku machozi yakianza kumlengalenga.
 

"Kusema kweli maisha ninayoishi na Mzee Yussuf hivi sasa ni tofauti na huko nyuma tulikotoka, Inaniuma sana,"alisema Khadija na kuangua kilio kikali.
 
Mapema Khadija alisema kuna kikundi cha watu ndani ya Jahazi, ambacho kimekuwa kikimchonganisha yeye na wifi yake, Leila Rashid, ambaye ni mke wa pili wa Mzee.


Alisema watu hao wamekuwa wakipeleka maneno ya umbeya kwa Leila wakidai kuwa yeye ndiye ameyasema na vivyo hivyo wamekuwa wakija kwake na kumweleza maneno kama hayo.
 

"Kuna wakati Leila amekuwa akinitumia meseji zenye maneno machafu, Ninapomjibu anakasirika Sielewi tunachogombea ni kipi,"alisema Khadija.
 

"Binafsi sina tatizo na Leila na sioni kwa nini tugombane, Sielewi na ninashangaa, Lakini hii yote ni kwa sababu kuna watu ndani ya Jahazi wanaotuchonganisha kwa makusudi,"aliongeza.
 

Kwa sasa, Khadija alikariri kuwa anajiandaa kuibuka na kibao chake kipya kitakachojulikana kwa jina la 'Na bado. '

Alisema kibao hicho kitazinduliwa katika onyesho maalumu litakalofanyika Desemba 30/31 mwaka huu. 

Hata hivyo juhudi zetu za kumtafuta Mfalme Mzee Yussuf au mkewe Malkia Leila Rashid zinaendelea kwa sasa ili tubaini yanayoendelea kati ya watatu hao.

Hii sio mara ya kwanza kwa wawili hao (Mzee Yussuf na dadake Khadija Yussuf) kukosana kiasi cha kunyimana salamu na kusemana vibaya kwenye vyombo vya habari, hali iliyomplekea Bi. Khadija kulikacha kundi la Jahazi linalomilikiwa na Mzee, kisha kwenda kushiriki kuanzisha Five Stars Modern Taarab na akiwa huko, alidaiwa kumpiga madongo mengi kaka yake katika miaka ya hivi majuzi.

Haya yanajiri huku bendi la Jahazi chini ya uongozi wake Mfalme Mzee Yussuf likijiandaa kuzindua rasmi albamu yao mpya ya tisa kwa jina la ‘Wasiwasi wako ndio maradhi yako’ tarehe 30/31 mwezi huu katika mkesha wa mwaka mpya huko Travertine Hotel, Magomeni Dar es Salaam Tanzania.

Additional reporting Toto la Matashtiti Mwa4.../Rusha Roho Blog

1 comment:

  1. wamejisumu wenyewe na nyimbo zao na vishindo vyao... uchawi huanzwa na aeen, jitho, sihir, mwisho kupewa jini

    ReplyDelete