Wednesday, 19 December 2012

KIBAO CHA 'WASIWASI WAKO NDIO MARADHI YAKO' CHAMTOA KIJASHO MZEE YUSSUF....

Hivi karibuni, Mfalme wa taarab, Mzee Yussuf alikuwa na kibarua kigumu wakati wa kurekodi wimbo wake mpya na kulazimika kuomba mapumziko kila dakika.

Wimbo huo “Wasiwasi wako” ambao utabeba jina la albam mpya itakayozinduliwa tarehe 30 mwezi huu, ulimpa shida Mzee Yussuf kutokana na jinsi ulivyo na njia nyingi za kupanda na kushuka na kumfanya Mfalme huyo wa taarab atumie nguvu nyingi za kusukuma sauti.

Mara kadhaa Saluti5 (mtandao wa burudani) ilimshuhudia Mzee akilazimika kukaa chini na kuugulia koo lake na kama si ukali wa Producer Bakunde, basi kazi hiyo ingeahirishwa kwa mara nyingine tena. 

Nyimbo 5 kati ya 6 zitakazounda albam hiyo zilishakamilika tangu wiki iliyopita, lakini Mzee Yussuf amekuwa mgumu wa kumalizia wimbo wake ambapo kila wakati alikuwa akiibuka na sababu kadhaa zikiwemo malaria na mafua. 

Hivi karibuni, Mzee alisema amefunga ‘sunna’ na ingemuwia vigumu kurekodi wimbo huo, lakini Bakunde alimwambia kwa jinsi ratiba yake ilivyo hapo studio, kama wangeshindwa kurekodi juzi basi ingemlazimu kuifanya kazi hiyo baada ya uzinduzi wa albam jambo ambalo lingekuwa halina maana kwa sababu Jahazi wanataka kuuza CD za nyimbo mpya siku ya uzinduzi.

Kutokana na hali hiyo, Mzee hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuingia studio na kurekodi wimbo wake, kazi ambayo ilijaa vituko, malalamiko na usumbufu mwingi kutoka kwa mkurugenzi huyo wa Jahazi.

“Wasi wasi wako” ni kazi nyingine itakayodhihirisha ubora wa Mzee Yussuf ambapo mbali na vionjo vya kuvutia, utakutana na ngoma za sindimba ndani yake hali itakayokufanya ushuhudie mapinduzi mengine ndani ya muziki wa taarab.

Nyimbo zingine zinazounda albam hiyo itakayozinduliwa katika ukumbi wa Travertine, Dar es Salaam ni pamoja na Mambo Bado (Khadija Yussuf), Kazi Mnayo (Mohamed Ali Mtoto pori), Nipe Stara (Rahma Machupa), Hata bado Hujanuna (Fatma Ali Mama Shughuli) na Sitaki Shari (Leila Rashid). 

Wakati huo huo kundi la Jahazi Modern Taarab linatarajiwa kufanya onyesho kubwa mjini Morogoro siku ya Mkesha wa X-Mas.

Mkurugenzi wa kundi hilo, Mfalme Mzee Yussuf, ameiambia Saluti5 (Mtandao wa burudani) kuwa onyesho hilo litakuwa ni mahsusi kwa ajili ya kuupima uzinduzi wao utakaofanyika jijini Dar es Salaam Disemba 31.

Onyesho la Morogoro litakuwa kama ndio ‘Listening Party’ yetu, tutapiga nyimbo zote za albam mpya na kuangalia namna zitakavyopokewa na mashabiki wa Moro na kisha baada ya hapo tutajua nini cha kupunguza au kuongeza kwenye onyesho letu la uzinduzi" alifafanua Mzee Yussuf. 

Wakazi wa Morogoro watashuhudia onyesho hilo siku ya Jumatatu ya tarehe 24 ndani ya ukumbi wa Savoy Hotel.

Na huku hayo yakijiri...Mwimbaji wa Jahazi Modern Taraab, Monica Robert, maarufu zaidi kama Mwasiti, anatarajiwa kufunga ndoa na mpenziwe Joseph Boimanda katika sherehe itakayofanyika baadae mwezi huu siku ya mkesha wa X-mas.

Hivi karibuni, kitchen Party yake ilifanyika katika ukumbi wa Kassa ulioko Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Mwasiti ambaye pia ni afisa utawala wa Jahazi, ni mtoto wa aliyekuwa mwimbaji maarufu wa TOT Taarab, marehemu Leila Khatib.

Courtesy of Salut5.....
 



No comments:

Post a Comment