Wednesday 19 December 2012

MOMBASA STARS KUIBUKA NA ALBUM MPYA MWAKA WA 2013.....

Bendi linalokuja kwa kasi sana mjini mombasa katika tasnia ya taarab yaani 'Mombasa Stars Modern Taarab' linajiandaa kuachia album mpya kwa jina la 'Nichombeze.'

Katika Mahojiano ya kipekee katika kipindi cha taarab kinachonoga kote mkoani pwani cha 'Kwa Raha Zangu kupitia Pwani FM, Sultan wa mirindimo Dr. Malik alipasua mbarika na kudokeza kuwa albamu hiyo itakuwa na vibao vinne ndani japo kwa sasa inaendelea kupikwa na itakamilika na kuzinduliwa mwaka wa 2013 panapo majaaliwa yake Mola.

Baadhi ya mistari katika kibao kitakachotambulisha album hiyo kwa jina la 'Nichombeze' kitakachoimbwa naye Dr. Malik ni,

"Nichombeze nichombezeke.... Mpaka vidughushi wakereke...Nnapenda raha zako zinanipa afya tele na pale nizikosapo hukonda kama unyelee....Nichombeleze kwa muala aaahh Niliwazeee miye....." 

Wakati huo huo, Dr. Malik aligusia hatma yake kwa sasa katika tasnia ya taarab na alisema,

"Mimi nipo katika muziki kama kawaida na nilitaka kuwatia tumbo joto kuwaangalia wale wapambe wasopenda tuwe katika sanaa lakini kutokana na upendo wa mashabik ndio kwa sasa tunaendelea na kazi ila sijajiondoa kama inavyosemekana," Akasema Dr. Malik.

Pia alididinda kuzungumzia kuhusu maisha yake ya kibinafsi ambapo inadaiwa kuwa ndoa yake ilikumbwa na msukosuko hivi karibuni hadi kupelekea kuachana na mkewe na kufikia sasa inadaiwa ameonekana akiwa na mpenzi mpya.

"Nisingependa kuyazungumzia hayo sababu sio muhimu ila ningependa tuzungumzie zaidi biashara wala sio maisha yangu binafsi," Akasema Dr. Malik. 

Haya yanajiri huku bendi hilo likishirikiana na lile la TOT likipanga kutambulisha album yao ya hivi karibuni ya 'Give us Time' kwenye tamasha la kufungwa mwaka litakaloandaliwa katika ukumbi wa Club Tropicana wakati wa mkesha wa mwaka mpya 2012/2013.

No comments:

Post a Comment