Monday, 10 December 2012

E.A MELODY IPO IMARA - HAJI MOH'D....

“Kundi la East African Melody bado lipo imara kama kawaidaaaaaa na lipo kikazi zaidi…”

Matamshi hayo ni kutoka kwake mkurugenzi wa bendi hilo Haji Mohamed akiwasuta vikali wale wanaodai  kuwa bendi hilo limefifia kiusanii katika tasnia ya taarab.

Akizungumza moja kwa moja katika kipindi cha taarab kinachotikisa mkoa mzima wa Pwani cha ‘Kwa raha zangu’ kupitia Pwani FM Mombasa Kenya, Haji alikariri kuwa kwa sasa bendi hilo linaendeleza mikakati ya kuzindua albamu yake mpya ya ‘Rabi Nilinde.’

“Nyimbo mpya zipo pamoja na zile za zamani ambazo zinatengenezwa, na kama sasa hivi tunakamilisha albamu yetu latest ya ‘Rabi Nilinde’ na tayari tumeshatengeneza nyimbo mbili ya ‘Rabi Nilinde’ iliyoimbwa na Mwanahawa Ali, ‘Stara’ iliyotiwa sauti na Swabaha Salum na nyimbo mbili ndio zimesalia na moja inayoitwa ‘Uke wenza sio deal’ itaimbwa na Mwanaidi Shaaban na ya mwisho itakuwa ya kujibizana ambapo hatujaipatia jina itakayoimbwa na Ramla Seif na Hafidh,” Anasema Haji Moh’d.

“Uzinduzi wa album ya ‘Rabi Nilinde’ hapo awali uliathirikika na msiba wa marehemu Mahmud Aalawy na ndio hapo tukazuia kazi karibu mwezi mzima na sasa tumerejea kazini na hivi tunajipanga kuzindua album hiyo pamoja na kuadhimisha miaka 20 ya bendi hili mwishoni mwa mwaka huu,” anasema Haji Moh’d.


Bwana Haji ambaye pia ni mmoja kati ya waimbaji katika bendi hilo hakusita kufafanua bifu lililokuwepo kati ya bendi la East African Melody na Gusagusa Mini Band,

“Kwa sasa hamna bifu lolote kati ya mabendi haya mawili ila Gusa Gusa ilitokana na Melody na mimi ndio niliokuwa mwanzilishi wa GusaGusa Mini Band na tulikuwa tukitumia vyombo vya Melody, ukumbi wa mazowezi wa Melody, Umeme na nguvu za Melody kufanyia kazi za Gusa Gusa Mini Band, lakini kutokana na tofauti zangu na kundi hilo ndio baadaye  nikajiengua na kurudi Melody na kusababisha sintofahamu lakini kwa sasa yameisha,” Anasema Bwana Haji Mohd.

Kuhusu bifu linaloendelea kati ya Bi. Mwanahawa Ali na Afua Suleiman Haji anasema kuwa,

“Tumefuatilia kwa sanaaa nini kinachoendelea kati ya wawili hao mpaka tumechoka ila sababu hatujazioni lakini wanajijua wenyeweee na tulipomsikia Bi. Afua kupitia vyombo vya habari na magazeti akitoa vitisho na maneno ya kihuni dhidhi ya Bi. Mwanahawa, tulimuonya na hakusikia na ndipo tulimchukulia hatua ya kumwandikia barua ya kutaka aeleze kamili kinachoendelea kati yake na bendi hili ili tutafute suluhu ya kudumu, mara tukasikia kajiingiza GusaGusa bila hata kufukuzwa,” Anasema Haji Moh’d.

Alipinga madai ya bendi hilo kumpendelea zaidi Bi.Mwanahawa Ali kikazi,

“Hatumpendelei isipokuwa Mwanahawa ni mtendaji mzuri wa kazi, na pia hatujamsikia akitoa maneno mabaya dhidhi ya Afua,” Akasema Haji Moh’d.

Wasanii waliosalia katika bendi hilo kwa sasa ni Bi. Mwanahawa Ali, Mwanaidi Shaaban, Haji Moh’d, Swabaha Salum (mara kwa mara), Zubeida Mlamali, Ramla Seif, Asina Soud, Maryam Hamdan, na Asya Hassan.

Na hatimaye Haji hakusita kutoa siri ya mafanikio ya bendi hili kwa kusema,

“Nidhamu na utendaji mzuri wa kazi, tunafanya kitu ambacho kinaeleweka na wapenzi wanafurahia kazi yetu na muziki wetu sisi unakwenda na kila rika ukilinganisha na bendi mingine, tunajaribu kulinda heshima, utamaduni, silka, mila na tamaduni za mtanzania.”

1 comment:

  1. melody wakubali wakatae washafulia...wakati wao ulikua si sasa tena...wametamba jamanitoka mi mdogo paka nimekua melody ilikua haina mpinzani..kuundwa zanzibar stars mwaka wa 2000 ndo chanzo cha kifo cha melody..na nyimbo zao paka leo zinautamu..ila hawawez kurudi tena kama awali...mtunzi wao gwiji Mahmoud Al-Alawy ndo huyo yupo mbele za haki alotunga maahsairi na mzika wa nyimbo nyingi zinazovuma paka leo hayupo tena..

    ReplyDelete