Sunday 23 December 2012

"MAMBO SHWARI KATI YANGU NA DADANGU" - MZEE YUSSUF....

Mfalme Mzee Yussuf amepinga vikali kuwa uhusiano kati yake na dadake Khadija Yussuf umekumbwa na mushkil kwa mara nyengine tena.

Akizungumza na Blogu hii moja kwa moja, Mzee amekiri kuwa uhusiano kati yake na dadake Bi. Khadija Yussuf uko imara wala hautawahi kuvunjika.

“Uhusiano kati yangu na dadangu bado uko imara wala hautawahi kuvunjika kama wanavyotaka wapambe,” Anasema Mzee Yussuf.

Haya yanajiiri baada ya Bi. Khadija Yussuf kupitia kipindi cha ‘Sham Sham za Pwani’ kinachorushwa kupitia runinga ya ITV kuangua kilio akidai kuna ‘Vidudu watu’ ndani ya bendi la jahazi wanaopeleka maneno ya urongo kwa kaka yake ili kuwagombanisha kiasi cha kuwafanya wasielewane vizuri.

"Kinachoniuma zaidi ni kwamba afadhali hayo maneno ningekuwa nimeyasema, lakini sijafanya hivyo, Hawa watu wanapaswa kutambua kwamba kuna Mungu na mimi na Mzee Yussuf tumezaliwa baba mmoja mama mmoja, atakapozikwa Mzee Yussuf ndipo nitakapozikwa mimi,"alisema Khadija huku machozi yakianza kumlengalenga.
 

"Kusema kweli maisha ninayoishi na Mzee Yussuf hivi sasa ni tofauti na huko nyuma tulikotoka, Inaniuma sana,"alisema Khadija na kuangua kilio kikali.

Mapema Khadija alisema kuna kikundi cha watu ndani ya Jahazi, ambacho kimekuwa kikimchonganisha yeye na wifi yake, Leila Rashid, ambaye ni mke wa pili wa Mzee.


Alisema watu hao wamekuwa wakipeleka maneno ya umbeya kwa Leila wakidai kuwa yeye ndiye ameyasema na vivyo hivyo wamekuwa wakija kwake na kumweleza maneno kama hayo.
 

"Kuna wakati Leila amekuwa akinitumia meseji zenye maneno machafu, Ninapomjibu anakasirika,  Sielewi tunachogombea ni kipi,"alisema Khadija.
 

"Binafsi sina tatizo na Leila na sioni kwa nini tugombane, Sielewi na ninashangaa, Lakini hii yote ni kwa sababu kuna watu ndani ya Jahazi wanaotuchonganisha kwa makusudi,"aliongeza.
 

Hata hivyo juhudi zetu za kumtafuta Malkia Leila Rashid zinaendelea kwa sasa ili tubaini yanayoendelea kati ya wawili hao.


No comments:

Post a Comment