Friday, 18 January 2013

MDOGO WAKE ALLY STAR ALIYETESEKA KITANDANI KWA MIAKA 8 AFARIKI DUNIA...

Ally Star....
MDOGO wake na mwimbaji wa TOT Taarab, Ally Hemed Star, amefariki jana jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
 
Marehemu aliyejulikana kwa jina la Abdallah Hemed, anategemewa kuzikwa Ijumaa ya leo asubuhi nyumbani kwao Kilosa mkoani Morogoro.

Ally Star ameiambia Saluti5 kuwa waliondoka Dar es Salaam jana jioni kwa gari la TOT, kuelekea Kilosa kumhifadhi mdogo wake mpendwa.

Kufariki kwa Abdallah Hemed ambaye ndiye anayemfuatia Ally Star kwa kuzaliwa, ni matokeo ya kuugua kwake ugonjwa wa kupooza uliomlaza kitandani kwa miaka minane.

Siku kadhaa zilizopita, Saluti5 ilifanya mahojiano marefu na Ally Star ambapo alizumgumzia jinsi maisha ya kumuuguza mdogo wake yalivyo.

Akimzungumzia mdogo wake wiki chache zilizopita kupitia Saluti5, Ali Star alisema: Kwa kujibana sana gharama za dawa kwa kila wiki ni sh.57,000, mwaka wa nane sasa anamhudumia mdogo wake ambaye anaishi nae nyumbani kwake.

“Pesa zinazoingia ni kidogo, zinazotoka ni nyingi, naumia sana kwa kumuona mdogo wangu anateseka kitandani, lakini naumia zaidi pale ninapohisi kuwa wakati fulani mi si msaada wa kutosha kwake.

“Wakati mwingine unatembea barabarani unaongea peke yako kama chizi, natamani siku moja nipate japo neno moja kutoka kwa mdogo wangu lakini Mungu alishamfunga kauli siku nyingi, hana uwezo wa kufumbua mdomo na kuongea lolote, tunatazamana kama picha tu.

“Maisha ya Hospital yameshindikana, kwasasa matibabu yote yanafanyika nyumbani, hata chakula chenyewe ana kula kwa mrija, kila siku hali inazidi kukatisha tamaa” hiyo ndio ilikuwa kauli ya Ally Star.

Ally Star ameiambia Saluti5 kuwa anaushukuru uongozi wa TOT, wasanii wenzake na wadau wote walifanikisha safari ya kwenda Kilosa kumzika mdogo wake.

Kwa hisani ya Saluti5....The screen masters.


No comments:

Post a Comment