Thursday 20 September 2012

NIPO JAHAZI NA NITASALIA KUWA JAHAZI – ASEMA BI. MIRIAM AMOUR NA FATMA KASSIM...

 
Ni msanii aliyetulia maishani na katika sanaa ya burudani, mcheshi asiyependa makuu wala kuwa na skendo za kiaina kama wasanii wengine katika tasnia ya taarab.

Ni mmoja katika ya wasanii waliotoka mbali kisanii, aliyetunukiwa kipaji cha hali ya juu na kuenziwa na umma mkubwa kwa mirindimo yake laini ya taarab kama ‘Sichoki kustahamili, Niepushie, Penye neema hapakosi husda’ miongoni mwa vibao vingine.

Si mwengine ila ni Bi. Miriam Amour kutoka bendi la jahazi Modern Taarab.

Bi. Miriam amefichua siri ya kutulia kwake katika bendi la jahazi, “Bado niko jahazi na nitasalia kuwa jahazi kwasababu bendi hilo linanikidhia mahitaji yangu kimalipo na kwa upande wa huduma pia, limenipa fursa ya kuonesha kipaji changu cha kuimba kwanini nihame? Wala sina nia hiyo kwa sasa,” anasema Bi. Amour.

Wakati huo huo Bi. Amour amesema hana kibao kipya katika album mpya ya jahazi inayojulikana kama ‘Wasiwasi wako ndio maradhi yako’ kwani ametoa nafasi kwa wasanii wenzake ambao ni machipukizi.

Safari yake bibi huyu ilianza katika bendi mbali mbali ikiwemo kundi la East African Melody na hadi sasa kusalia katika bendi la Jahazi.

Mbali na sanaa ya burudani, Bi. Amour ni mfanyibiashara na ni mke nyumbani na mama wa watoto wawili.

Bi. Amour alibahatika kuolewa tena hivi karibuni baada ya kuachika kwa muda.

Huku hayo yakijiri….Fatma Kassim kutoka bendi la Jahazi ambaye ni dadake Jokha Kassim amesema bado yupo katika bendi hilo wala hana mipango ya kuhamia bendi lingine kwani sababu hajaiona.

Bi. Fatma alijipatia umaarufu katika tasnia ya taarab kutokana na kile kibao chake ‘Hakuna mkamilifu’ katika album ya 6 ya jahazi inayoitwa ‘Wagombanao ndio wapatanao.’

Fatma amesema uhusiano wake na dadake Jokha Kassim kutoka bendi la T Moto uko shwari na kila mmoja anaendelea na kazi kivyakevyake.

Haya yanajiri huku mabadiliko makubwa yakiendelea kufanywa katika bendi la jahazi, hatua itakayopelekea baadhi ya wasanii kujipatia nafasi na wengine kuhama bendi hilo .

No comments:

Post a Comment